Andiko hili ni maalum kwa ajili ya Wanafunzi wetu Wanaojifunza Uwekezaji kupitia Akademi ya Uwekezaji ya HAIPPA kuwapa fursa ya kufahamu Hisa inajengaje utajiri wa Mwekezaji.
Coca Cola ilianzishwa mwaka 1882 na Mfamasia John Pemberton. Baadaye John Pemberton aliuza kanuni ya kutengeneza kinywaji hicho kwa mfanyabiashara Asa Griggs Candler ambaye mwaka 1892 iliisajili Coca cola kuwa Kampuni. Mwaka 1919 Candler aliiuza hisa za Kampuni ya Coca Cola kwenye Soko la Hisa la New York kwa mara ya kwanza kwa thamani ya $25milioni ambapo kila hisa iliuzwa kwa $40. Mwaka 1926 hisa ya coca cola ilipanda bei na kuuzwa hadi $170 kampuni ikalazmika kufanya kitu kinaitwa share split.
Share split ni kitendo cha kuvunja hisa katika vipande vidogo zaidi bila kupoteza thamani yake.Hii hufanyika kimkakaati ili kuzifanya hisa za kampuni kuendelea kununulika kwa urahisi. Mpaka sasa hisa za Coca cola zimeshavunjwa mara 11 na kuifanya hisa moja iliyonunuliwa mwaka 1919 leo kuwa na thamani sawa na hisa 9200 huku hisa moja leo ikiwa inauzwa kwa $64. Hii Ina maana Mtu aliyenunua Hisa Moja Mwaka 1919 kwa $40 Leo zimejizaa na kuwa Hisa 9200 zenye thamani ya $588,800 sawa na Tshs 1.472 Bilioni
Mambo 10 ya kujifunza kutoka kwenye mwenendo huu wa Hisa ya Coca cola kwenye Soko la Hisa la New York:
- Hisa yenyewe kama hisa ni pesa. Mfano hisa moja iliyonunuliwa mwaka 1919 imeendelea kujizaa na leo imefika hisa 9200. Ikimaanisha mtu aliyenunua hisa moja ya Coca cola mwaka 1919 kwa $40 leo ana hisa 9200 za Coca cola zenye thamani ya $64 kila moja.
- Hisa inajenga utajiri bila jasho. Kwamba kama wakoloni waliokuwa wanaitawala Tanganyika wakati huo wangewanunulia kila familia au kaya (yenye watu 5) ya Mtanganyika Hisa tano tu za Coca Cola mwaka 1919 (kadiria zilikuwa kaya 200,000) leo hizo kaya 200,000 kila kaya ingekuwa na utajiri wa $2,944,000 (Sawa na Tshs 7.36 Bilioni ) na kama ukwasi huo ukigawanywa kwa watanzania wote leo wastani kila Mtanzania angekuwa na ukwasi wa Tshs 22,646,000
- Hisa inarahisisha mgawanyo wa utajiri. Kwa kupitia hisa leo ni rahisi sana kufahamu utajiri wa kila mwanahisa wa Coca Cola bila kutumia nguvu kubwa wala jasho.
- Hisa inarahisisha kurithisha utajiri. Wengi wa wawekezaji walionunua hisa za Coca Cola wakati zilipouzwa kwa mara ya kwanza huenda hawapo lakini warithi wao wameendelea kufaidi uwekezaji huo mpaka leo.
- Hisa inarahisha uhamishaji wa umiliki bila kuathiri uchumi wala biashara ya Kampuni. Inawezekana wengi wa walionunua hisa za Coca Cola wakati zikiuzwa kwa mara ya kwanza walishauza hisa zao na inawezekana kuna ambao umiliki wa hisa umebadilika hata mara kumi. Jambo kubwa hapa ni kwamba uhamishaji wa umiliki huo una athari ndogo sana au hauthiri kabisa Uchumi wala biashara ya kampuni.
- Hisa zinakuza uchumi wa nchi. Leo Coca Cola ni global company kwa maana ya kampuni inayofanya biashara kila mahali duniani kwahio popote unapokunywa kinywaji cha Coca Cola au popote kinaponyweka kinywaji cha Coca Cola unachangia uchumi wa mwanahisa wa Coca cola na uchumi wa Taifa la Marekani.
- Hisa zinajenga Kampuni kubwa. Kwa njia ya Hisa imekuwa rahisi kuijenga kampuni ya Coca Cola kuwa kampuni ya dunia (a global brand)
- Hisa zinaifanya Kampuni kuwa mali ya watu wote. Kwa kuwa Coca Cola ni kampuni ya Umma, ina maana mtu yeyote leo anaweza kununua hisa za Coca Cola na kuwa sehemu ya wamiliki na wanufaika. Hali hii inaifanya Kampuni ya Coca Cola kuwa sio kitu cha mtu mmoja bali kitu cha watu wote.
- Hisa zinaifanya Kampuni kuwa mlipakodi mkubwa hivyo kuvuta umakini wa Serikali kwa kampuni. Ni nadra sana kusikia kampuni ya umma imetaifishwa.
- Tafadhali tuambie wewe unaona faida gani nyingine na unajifunza nini kutoka kwenye Mwenendo wa Hisa za Coca Cola?
Unataka kujifunza zaidi na kuwekeza na HAIPPA PLC jaza fomu yetu: https://in.haippa.co.tz/authentication/signup
Mwandishi wa Makala hii ni:
CPA. Boniface Ndengo
Mkurugenzi Mkuu
HAIPPA PLC
Afrika Investment Academy